HALMASHAURI ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro inatazamia kutumia zaidi ya shilingi milioni 30 kwa ajili ya kuboresha utendaji wa kazi ya kusimamia shughuli za lishe ngazi ya jamii.
Fedha hizo ambazo zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019 /2020 zitasaidia ufuatiliaji na utoaji wa elimu ya lishe ili kuhakikisha kuwa jamii nzima ya wilaya ya Hai inakuwa na afya njema na kuondokana na magonjwa yanayosabaishwa na ukosefu wa lishe.
Akizungumza na watendaji wa kata na vijiji katika kikao kazi cha kuweka mkataba wa utendaji kazi na usimamizi wa shughuli za lishe ngazi ya jamii wilayani Hai, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Yohana Sintoo , amesema kuwa halmashauri imejipanga kuhakikisha kuwa inatoa elimu ya kutosha kwenye jamii kwa kupitia viongozi waliopo kwenye maeneo yao.
Amefafanua kuwa zoezi la utoaji wa elimu kwa ajili ya lishe , litafanyika kwa ngazi zote lengo ikiwa ni kufikia wananchi kuanzia nagzi za vitongoji hali ambayo itasaidia kuondoa utapiamlo unaosababishwa na upungufu wa virutubisho au kuwa na wingi wa virubisho kupita kiasi mwilini.
Kwa upande wake Afisa Lishe wilaya ya Hai, Silvania Ignace amesma kuwa lengo la mpango huu ni kuhakikisha jamii kupitia viongozi wao kwa pamoja wanashiriki ipasavyo katika kupanga na kutekeleza kufuatilia maendeleo ya kazi za lishe na malezi ya watoto.
"Viongozi wa kata hakikisheni kuwa wadau wa lishe wote waliopo kwenye kata wanatambulika na wanawasilisha taarifa zao kwenye kamati za kata pamoja na kuhakisha kuwa wanafanikisha hali lishe na kupunguza athari za utapiamlo kwenye jamii”amesema
“Naombeni sana katika vikao vyenu kwenye vijiji kuhakikisha kuwa mnatoa taarifa za lishe kila robo ya mwaka ili kuweza kujua mafanikio yanayopatikana katika zoezi hili ” amesema Ignace.
“Pia napenda kuwakumbushia wahudumu wa afya ya jamii wahakikishe wanatembelea kaya na kutoa elimu ya lishe, Afya uchangamshi maji na usafi wa mazingira na vilevile kila kijiji kushirikiana na vituo vya kutolea huduma za afya katika zoezi la utoaji wa nyongeza ya vitamin kwa watoto wenye umri wa miezi 6-59” amefafanua afisa huyo.
Awali akifungua kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, Katibu Tawala wa wilaya, Upendo Wella amewataka watendaji hao kuhakisha wanatoa ushirikiano katika utekelezaji wa mkataba waliosaini ili kuhakikisha kuwa jamii inakuwa na afya bora kwa kuzingatia mambo yaliyoorodheshwa kwenye mkataba.
“Watendaji wa vijiji na kata wamehusishwa moja kwa moja wakawe wajumbe au wasimamizi kuhakikisha jamii ambazo wanaziongoza zinakuwa na lishe bora” amesema Wella.
Wilaya ya Hai kwa sasa ina asilimia 29 ya watoto wanaokabiliwa na tatizo la udumavu wa lishe jambo ambalo wameliwekea mikakati ya kuondoa tatizo hilo.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai