Wito umetolewa kwa waandikishaji wa huduma za bima ya afya ya jamii (ICHF) kuwaelimisha wananchi wanaowaandikisha ili kuimarisha uelewa wa wanajamii na kuondoa dhana potofu inayoenezwa kuhusu huduma za bima hiyo.
Akizungumza kwenye mafunzo ya kuwaongezea uwezo waandikishaji wa bima hiyo katika Wilaya ya Hai; Meneja Mradi kutoka Tume ya Kikrito ya Huduma za Jamii (CSSC), Godlisten Moshi amesema waandikishaji wanatakiwa kuzungumza na wananchi wanaowaandikisha na kuwaelimisha kwa undani kuhusu huduma zinazotolewa na bima hiyo.
Moshi amewataka waandikishaji kuwaelimisha wananchi kuhusu aina ya huduma ambazo hazitolewi na mfuko huo ili wawe na uelewa wa huduma hizo na kuwafanya wasihuzunike pale wanapokosa aina hizo za huduma.
Naye Mratibu wa Bima hiyo katika Wilaya ya Hai Elia Kapinga amesema waandikishaji waendelee kuwa daraja la kufikisha wilayani taarifa za changamoto wanazokutana nazo wananchi katika kupata huduma ili kuwasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto hizo.
Aidha Kapinga amewakumbusha waandikishaji kutekeleza majukumu yao hasa kazi ya kuwasajili wananchi kwenye mfumo wa bima ili kuwafikia watu wengi Zaidi na kuwa na bima imara lakini pia kuwa na jamii yenye afya na uhakika wa kupata matibabu pale wanapougua.
Kwa nyakati tofauti waandikishaji walioshiriki mafunzo hayo wameshukuru uongozi wa wilaya kwa kuandaa mafunzo hayo kwani elimu waliyoipata itawasaidia kuboresha utendaji wao lakini pia itawasaidia kutoa elimu sahihi kwa wananchi wanaowahudumia.
Mafunzo haya ya kuwaongezea ujuzi waandikishaji ni moja kati ya mbinu kadhaa zinazotumiwa katika kuwafikia wananchi wengi Zaidi ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa kutumia mifumo ya bima nafuu kwa wananchi.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai