Chama cha ushirika wa Akiba na Mikopo cha waalimu wilaya ya Hai na Siha (HAI RURAL TEACHERS SACCOS) Mkoani Kilimanjaro leo kimetoa Msaada wa Vifaa mbalimbali Vyenye thamani ya Sh.milioni 2 katika hospitali ya Wilaya ya Hai vitakavyowasaidia wahudumu wa afya katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Mwenyekiti wa chama hicho Terewandumi Swai amesema kuwa chama hicho ni sehemu ya Jamii hivyo Kila mwaka kimeweka utaratibu wa kushiriki katika mambo ya kijamii ili kutekeleza msingi mmojawapo wa ushirika wa kuijali jamii.
Amesema kuwa kutokana na Taifa kuendelea kukabiliana na janga la COVID 19, mwaka huu wameona ni vyema kuiunga serikali mkono katika mapambano hayo kwa kuwasaidia mahitaji muhimu wahudumu hao wa afya ambao wakati wote wamekuwa wakiwahudumia wagonjwa.
Naye Meneja wa Chama hicho Upendo Lyatuu ametoa rai kwa vyama vingine vya ushirika kushiriki katika kuisaidia serikali na jamii kwenye mapambano dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa COVID 19.
Akizungumza wakati akipokea mchango huo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai Dkt. Irene Haule amewashukuru wanachama wa chama hicho kwa mchango huo huku akiwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari mbalimbali zinazoelekezwa na wataalamu wa afya katika kujikinga na maambukizi virusi vya Corona kwani bado ugonjwa huo upo na pia bado wilaya ya Hai ina wagonjwa wa virusi hivyo ambao bado wanaendelea kupatiwa matibabu.
Mchango uliyotolewa na chama hicho na kukabidhiwa kwa Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo ni pamoja na Vitakasa mikono (Sanitizers) lita 100, Mchele kilo 100 na mafuta yakupikia lita 30 vyote vyenye thamani ya shilingi milioni 2.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai